Vidokezo vya Kupata Kazi

Fahamu njia mbalimbali za kupata kazi Tanzania, pitia tovuti na blogu kama njia rahisi ya kupata taarifa juu ya nafasi za Ajira Tanzania, fahamu yote haya kupitia mywage.org/Tanzania

Vidokezo vya namna ya kutafuta na kuomba kazi Tanzania

Napataje kazi Tanzania?

Ukiwa Tanzania unaweza kutafuta kazi kwa kutumia njia zifuatazo:

•    Kupitia vyombo vya Habari; kwa mfano magazeti, tovuti na blogu ambazo ni mashuhuri kwa kutangaza matangazo mbalimbali.

•    Kwa kupitia mara kwa mara tovuti za makampuni ambayo ungependa kufanya nao kazi. Makampuni mengi huweka matangazo ya nafasi za kazi katika tovuti zao na sio lazima katika magazeti. Ni muhimu kua na mazoea ya kutembelea tovuti mbalimbali mara kwa mara, hii itaongeza nafasi yako ya kupata kazi.

•    Kupitia marafiki na jamaa ambao wanaweza kukupatia taarifa muhimu kuhusu nafasi za kazi na pia kukushauri wapi pa kupeleka maombi ya nafasi za kazi.

•    Kwa kutumia mawakala wa kuajiri kama vile Radar Recruitment, Kazi Services Ltd na wengineo. Kwa kawaida mawakala hawa hua na tovuti ambazo mtu hujiandikisha na kutuma CV yake kwa mtandao baada ya kuchagua aina za kazi ambazo ungependelea kufanya. Kumbuka kuweka mawasiliano yako ili kukuwezesha kupata nafasi.

•    Tembelea pia mawakala wa ajira wa Taifa kama vile TeSA ( Wakala wa huduma za ajira Tanzania) kwa taarifa juu ya nafasi za kazi zilizopo.

•    Pia waweza tembelea moja ya makampuni ambayo ungependa kufanya kazi na kuomba kuongea na meneja rasilimali watu au hata Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni pale inapowezekana. Unaweza kutuma barua ya kuomba kazi pamoja na CV yako kwa makampuni haya. Hii inaweza kua njia mbadala kwa kuzingatia kwamba mara nyingi inakua ngumu kuwaona hawa watu.

Ni vipi nitaomba kazi?

 Unapokua na taarifa za kutosha juu ya uwepo wa nafasi za kazi ambazo zinakidhi sifa zako au unataka kuomba hata bila ya kutangazwa kumbuka kufanya yafuatayo:

•    Tuma barua ya kuomba kazi yenye taarifa muhimu kama ilivyoelezwa katika dokezo la kuandika barua za kuomba kazi. Barua hii iambatanishwe na CV ili kuweza kumpatia mwajiri mtarajiwa taarifa zote za muhimu kukuhusu. Ukimaliza haya subiri kwa kipindi Fulani, mara nyingi utaitwa kwenye usahili.

•    Hakikisha unatuma barua na CV yako katika anuani sahihi. Anuani hizi hutolewa wakati nafasi za kazi zinavyotangazwa au pia unaweza kupata katika tovuti ya kampuni husika au hata katika vipeperushi vya kampuni husika. Kama nafasi haikutangazwa unaweza kupiga simu kufuatilia kama walipokea maombi yako na kama kuna utaratibu wowote unaoendelea.

•    Hakikisha CV yako ni fupi na yenye taarifa zote muhimu zinazohitajika. Taarifa hizi ni muhimu zikawepo katika ukurasa wa kwanza wa CV yako.

•    Tengeneza barua yako kwa kuweka msisitizo katika ujuzi ambao unawiana na mahitaji ya kazi iliyotangazwa.

•    Andaa makabrasha yako yote yatakayosindikiza maombi yako kama vile, vyeti vya shule na barua za wadhamini. Ni vizuri ukawa na nyaraka hizi katika mfumo wa picha kwa kuscan ilikukuwezesha kufanya maombi kwa kupitia mtandao. Kama utascan hakikisha unahifadhi nyaraka zako katika mfumo wa PDF.

Kutuma maombi yako kwa barua pepe

•    Hakisha unatumia anuani yako binafsi ya barua pepe au ya mtu wako wa karibu sana, hii itasaidia katika kupata majibu kwa wakati.

•    Kila mara tuma barua, CV na vyeti vyako kama ujumbe mmoja wa barua pepe na viambatanisho vyake. Ni vizuri kua na orodha ya vitu vyote muhimu unavyotakiwa kufanya wakati wa kutuma maombi ya kazi. Soma tena na tena kuepuka makosa. Kabla hujabonyeza kitufe cha kutuma soma tena kuepuka makosa.

•    Ukishatuma subiri majibu sasa. Hakikisha namba yako ya simu na njia nyingine za mawasiliano ulizoweka katika CV yako zinapatikana wakati wote toka utume maombi yako.

Loading...