Likizo ya Mwaka - Kimataifa

likizo ya mwaka yenye malipo ni kipindi katika mwaka ambapo mfanyakazi hupumzika na kazi zao lakini huku wakiendelea kupata mshahara wao na mafao mengine. Likizo ya mwaka yenye malipo ni tofauti na likizo ya kuumwa, likizo ya uzazi, siku za sikukuu n.k, fahamu yote haya kupitia mywage.or.tz

Ni ipi likizo ya mwaka yenye malipo?

Likizo ya mwaka yenye malipo ni kipindi Fulani katika mwaka ambapo mfanyakazi anapumzika na kazi huku akiendelea kupata malipo yake na mafao mengine kama vile yupo kazini. Likizo ya mwaka ni tofauti na siku za mapumziko za mwisho wa wiki ama siku za sikukuu, likizo za kuumwa na likizo za uzazi kwa mwanamke au mwanaume.

Kwanini kunakuepo na likizo ya mwaka?

Likizo ya mwaka yenye malipo inakuepo kwa sababu kuu mbili. Sababu ya kwanza ni kutoa fursa ya kupumzika kwa mfanyakazi. Pili kuwapa wafanyakazi fursa ya kukaa na familia zao kwa ukaribu zaidi ambayo inaboresha usawa wa kazi na maisha. Vile vile likizo hizi ni muhimu kwa afya ya mfanyakazi na hivyo kupunguza utoro kazini na gharama za matibabu.

Je Shirika la Kazi Duniani (ILO) linasemaje kuhusu likizo ya mwaka yenye malipo?

Shirika la Kazi Duniani (ILO) limekua na maazimio mengi kuhusiana na likizo ya mwaka yenye malipo ijapokua azimio jipya na la karibuni ni azimio la 132 ambalo linamtaka kila mfanyakazi aliefanya kazi kwa angalau mwaka mmoja kupata likizo ya angalau wiki 3 yenye malipo. Mfanyakazi aliefanya kazi kwa kipindi kifupi au kisichotimia mwaka 1 anastahili likizo fupi ya mwaka yenye malipo ambayo ina uwiano na kipindi alichofanya kazi. Kwa mfano, kama sheria za nchi zinatoa wiki 3 za likizo ya mwaka yenye malipo kwa mfanyakazi aliefanya kazi kwa angalau mwaka 1 basi mfanyakazi aliefanya kazi kwa kipindi cha miezi 8 anastahili angalau wiki 2 za likizo ya mwaka yenye malipo.

Ni kipi kiwango cha chini cha muda cha kufuzu likizo ya mwaka yenye malipo kilichoelezewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO)?

Nchi zinaweza kuweka kiwango cha chini cha muda wa kufanya kazi ambapo mfanyakazi atafuzu kustahili likizo ya mwaka yenye malipo. Kiwango hiki ni vizuri kikapangwa na taasisi inayohusika na masuala ya ajira na kisizidi miezi 6. Hata hivyo kama mfanyakazi atakua nje ya ofisi kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake kama vile magonjwa, kuumia au uzazi kipindi hicho kitahesabiwa kama alikua kazini.

Je ILO inasisitiza likizo ya mwaka yenye malipo?

Ndio, maazimio ya ILO yanahitaji mfanyakazi atakae chukua likizo ya mwaka alipwe angalau mshahara wake wa kawaida kwa kipindi chote cha likizo yake.

Je wafanyakazi wanaweza kuchukua likizo yao ya mwaka kwa mafungu?

Ndio, maazimio ya ILO yanasema kwamba taasisi inayohusika na masuala ya ajira katika nchi inaweza kuruhusu kuchukua likizo ya mwaka kwa mafungu. Ijapokua mafungu hayo ni lazima mojawapo liwe na angalau wiki 2 zisizo na usumbufu. Vile vile likizo ya mwaka inaweza kulimbikizwa hatahivyo ni lazima ichukuliwe ndani ya miezi 18 ya kipindi kinachostahili.

Ni nani anaamua wakati wa kwenda likizo ya mwaka yenye malipo?

Kama muda haujapangwa na kanuni au makubaliano ya pamoja basi muda wa kuchukua likizo ya mwaka yenye malipo huamuliwa na mwajiri baada ya kuongea na mfanyakazi wake au wawakilishi wa wafanyakazi. Hii itazingatia mahitaji ya kazi ( na mwajiri) na fursa za kupumzika na kustarehe zilizopo kwa mfanyakazi.

Je mfanyakazi anaweza kuchukua fidia ya likizo badala ya kwenda likizo?

Kutokana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), makubaliano ya kubadilisha likizo na malipo au kuuza likizo ni makubaliano yasiyo tambulika. Ijapokua kama mfanyakazi ambaye anastahili likizo yake ya mwaka yenye malipo atafutwa kazi basi anastahili kulipwa fedha sawa na siku zake za likizo alizokua anastahili kama hakuchukua likizo yake katika hicho kipindi. Mfanyakazi ambaye yupo kwenye likizo ya mwaka yenye malipo haruhusiwa kujihusisha na shughuli za kumwingizia kipato katika likizo yake.

Je sikukuu za kitaifa au kidini zinazotokea wakati wa likizo ni sehemu ya likizo?

Sikukuu za kitaifa ama kidini zinazoangukia ndani ya likizo ya mwaka yenye malipo hazihesabiwi kama sehemu ya likizo. Vile vile kipindi cha kushindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa au kuumia hazihesabiwi kama sehemu ya likizo ya mwaka yenye malipo.

Je mfanyakazi atapewa malipo ya awali kwa ajili ya likizo ya mwaka yenye malipo?

Kutokana na ILO, mfanyakazi anaechukua likizo ya mwaka atahitajika kuchukua angalau mshahara wake wa kawaida kwa kipindi cha likizo kabla haijaanza.

Ni vipi vielelezo vya kimataifa kuhusu likizo ya mwaka yenye malipo?
Likizo za mwaka zenye malipo ukilinganisha kimataifa ziko kati ya siku za likizo 10-15 kwenda 24-26. Stahili kubwa za likizo kwa kawaida zinapatikana katika bara la Ulaya wakati nchi za Asia ziko katika siku chache.
Kiwango cha chini cha kustahili likizo ya mwaka yenye malipo hakitumiki kwa wafanyakazi wote kwani wafanyakazi wanaoajiriwa kwa kipindi cha muda mfupi wanatolewa katika stahili hizi. Sheria za kazi kwa kawaida zinamtaka mfanyakazi awe amemaliza kipindi cha kufuzu cha miezi 6 au mwaka 1.
Katika nchi nyingine, likizo ya mwaka yenye malipo inaongezeka na nafasi ya kazi kazini. Wafanyakazi wenye uzoefu wa muda mrefu wa kazi wanapata stahili za muda mrefu za likizo. Jedwali hapo chini linatoa taarifa juu ya stahili za likizo ya mwaka katika nchi zinazotekeleza  mradi wa “ Haki za Kazi kwa Wanawake”.

NchiUtoaji wa likizo ya mwakaKipindi cha kufuzu
Misri Siku 21 kwa mwaka, stahili za ziada kwa waliofanya kazi muda mrefu au kazi ngumu na za maeneo ya pembezoni Miezi 6 ya kufanya kazi na mwajiri
Guetamala Angalau siku 15 kwa mwaka Angalau siku 150 za kufanya kazi na mwajiri
India Siku 21 kwa kila siku 240 za kufanya kazi Angalau siku 240 au zaidi za kufanya kazi na mwajiri
Indonesia Siku 12 kwa mwaka Miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
Kenya Angalau siku 21 za kazi Miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
Mozambique

1.) Siku 12 kwa kipindi cha  mwaka mmoja wa kazi

2.) Siku 24 kwa kipindi cha miaka 2 ya kazi

3.) Siku 30 kwa kipindi cha miaka 3 au zaidi ya kazi

Miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
Pakistani Siku 14 ukichanganyana na siku za kupumzika kwa wiki Miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
Paraguay

1.) Siku 12 mfululizo kwa mfanyakazi aliefanya kazi chini ya miaka 5

2.) Siku 18 mfululizo baada ya miaka 5 lakini pungufu ya miaka 10 ya kazi

3.) Siku 30 baada ya miaka 10 mfululizo ya kazi na kuendelea

Miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
Peru Siku 30 kwa mwaka Miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
South Africa Siku 21 mfululizo Mzunguko mmoja wa likizo ambao ni sawa na miezi 12 ya kufanya kazi na mwajiri
Chanzo cha taarifa hizi: Taarifa za ILO juu ya hali za sheria za kazi na ajira, ILO Geneva

Angalia Likizo ya mwaka - Tanzania

Jaza tafiti ya mishahara kuweza kuboresha taarifa za mishahara katika tovuti yako

Loading...