Ajira kwa Watoto

Fahamu kuhusu ajira kwa watoto, ni nini sheria inaseme kuhusu ajira kwa watoto na adhabu kwa mtu atakaeajiri watoto katika kazi zake, fahamu pia sheria inamuelezea vipi mtoto, je mtoto ni mtu wa aina gani? yote haya na zaidi kupitia www.mywage.org

Je Sheria za kazi zinamuelezea vipi mtoto?
Kifungu cha 4 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka, 2004 kinamuelezea mtoto kama mtu mwenye umri chini ya miaka 14 isipokuwa kwa ajira zilizo katika sekta hatarishi,  mtoto maana yake ni mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18.

Je kuna sheria yeyote inayosimamia ajira kwa watoto?
Ndio, kuna sheria kadha wa kadha zinazoelezea ajira kwa watoto kama vile katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sheria ya Watoto na sheria ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi zikiwa ni miongoni mwa nyingi. Lakini linapokuja suala la ajira na kazi, Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 ndio inayokidhi hasa.

Je kuajiri mtoto inakubalika kisheria?
Kwa ufupi sheria inakataza mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 kuajiriwa. Sheria pia inaendelea kukataza ajira kwa watoto chini ya miaka 18 katika maeneo ya migodi, viwanda, kama mabaharia katika meli au kazi nyingine yeyote inayotambulika kua hatarishi. Hata hivyo, sheria inaruhusu ajira kwa watoto wa miaka 14 katika kazi nyepesi ambazo sio hatarishi kwa afya ya watoto na maendeleo na haihatarishi mahudhurio ya watoto shuleni, ,mafunzoni au programu za kujifunza. Kwa ujumla ustawi wa watoto hautakiwi kuhatarishwa hata kidogo.

Je kuna adhabu kwa mtu atakayeajiri watoto kinyume cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004?
Ni kosa kuajiri watoto kinyume na sheria ya kazi inavyosema na adhabu inatolewa chini ya kifungu cha 102 (2) ambacho kinampaHakimu wa Wilaya na Mkazi kutoa adhabu sawa na faini isiyozidi shilingi milioni 5 au kifungo cha mwaka mmoja au vyote faini na kifungo kama mahakama itavyoona inafaa, kutegemea na mazingira ya kesi yenyewe.

Ni vipi Waajiri watafahamu kua maeneo yao ya kazi ni hatarishi?
Sheria inamtaka Waziri kuandaa orodha ya sekta hatarishi na kuisambaza kwa umma. Kwa sasa kuna rasimu ya orodha hiyo kutoka kwa Waziri wa Kazi na Ajira lakini bado haijasambazwa na kua rasmi.

Je mwajiri atakua na makosa kwa kuajiri mtoto kwa kupewa taarifa zisizo sahihi au kutotambua?
Kama mwajiri atatoa madai kwamba hakufahamu kwamba mtu aliyemuajiri ni mtoto wakati wa kumpa ajira au kudai kupewa taarifa zisizo sahihi watakua na wajibu wa kuthibitisha kua ilikua sahihi kwa wao au mtu mwingine yeyote mwenye akili timamu kuamini kwamba mtoto huyo  alikua na umri wa kuajiriwa. Ni lazima waonyeshe kwamba kulikua na hatua za kutosha kuhakikisha hawaajiri watoto. Uthibitisho wa cheti cha kuzaliwa, kumbukumbu za usahili na wazazi wa mtoto na uthibitisho mwingine wowote kuonyesha kwamba walipotoshwa, hii itawasaidia kuwaepusha na adhabu iliyotajwa hapo juu.

Je mtu atakua na makosa kwa kukuwadia mtoto kwa ajira?
Sheria inakataza kuajiri mtoto na kukuwadia mtoto kwa ajira. Kama kutakua na uthibitisho kwamba kulikua na ukuwadi wa watoto kwa ajira basi mtu huyo atakua na makosa na atachukuliwa hatua sawa na Yule aliyeajiri mtoto au watoto katika maeneo yake ya kazi.

Loading...