Mikataba ya Ajira

fahamu yote kuhusu mikataba ya ajira Tanzania, sheria za mikataba ya ajira, aina ya mikataba ya ajira, taarifa ya maelezo ya maandishi, mkataba wa maneno, mkataba wa maandishi, sheria ya ajira na mahusiano ya kazi ya mwaka 2004, fahamu yote haya kupitia Mywage Tanzania

Ni sheria gani inayosimamia mikataba ya ajira Tanzania?
Kwa ujumla Sheria ya Mikataba inasimamia aina zote za mikataba Tanzania. Lakini kwa mikataba mahususi kuna sheria mahususi inayosimamia mikataba hiyo. Kwa mfano Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi inaelezea mikataba ya ajira. Kwa maana hiyo ni sawa kusema Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi  ya mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Mikataba zote zinasimamia mikataba ya ajira.  


Kuna aina ngapi za mikataba?

Kuna aina kuu tatu (3) za mikataba ambazo unaweza kuajiriwa nayo, nazo ni:
•    Mkataba kwa kipindi cha muda usiotajwa: Kama jina linavyojieleza, kwa aina hii ya mkataba kipindi cha ajira hakiainishwi. Mara nyingine huitwa mkataba wa kudumu.

•    Mkataba kwa kipindi cha muda kilichotajwa: Hii ni aina ya mkataba ambao umetaja kipindi cha muda. Chini ya mkataba huu kama kipindi kilichotajwa kikimalizika basi mkataba utakua umefikia mwisho. Mkataba wa kipindi cha muda uliotajwa unaweza kua kwa kipindi cha mwezi, miezi mitatu, mwaka mmoja, miaka miwili nakadhalika.

•    Mkataba wa kazi maalumu: Hii ni aina ya mkataba ambapo mtu huajiriwa kufanya kazi maalumu. Pindi kazi inapoisha na mkataba hufikia mwisho.  Kwa mfano, mtu anaweza kuajiriwa kushusha kreti za soda kutoka kwenye gari na pindi kazi ile inapoisha na mkataba hufikia mwisho.

Kama mhasibu ama mtu wa fani nyingine naweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi cha muda kilichotajwa?
Ndiyo, Kutokana na kifungu cha 14 (1) (b) mkataba wa kipindi cha muda kilichotajwa ni kwa kada za wataalamu na mameneja. Ijapokua suala hili bado linalalamikiwa mara kwa mara kwani hauwezi kuajiri mtu ambae sio mtaalamu katika misingi hii. Sheria inaeleza kwamba wanatakiwa waajiriwe chini ya mkataba wa kazi maalumu au mkataba wa kipindi cha muda kisichotajwa/mkataba wa kudumu.

Ni nini taarifa ya maelezo ya maandishi na inahusisha vitu gani?

Taarifa ya maelezo ya maandishi ni  orodha ya taarifa kuhusu mfanyakazi ambayo lazima mwajiri ampatie mfanyakazi pindi mfanyakazi anapoanza kazi. Taarifa ya maelezo ya maandishi ni lazima iwe na taarifa zifuatazao kuhusu mfanyakazi:

•    Jina, umri, anuani ya kudumu na jinsia ya mfanyakazi
•    Mahali alipoajiriwa
•    Kazi yake
•    Tarehe ya kuanza
•    Muundo na muda wa mkataba
•    Kituo cha kazi
•    Saa za kazi
•    Ujira(mshahara), njia za ukukotoaji wake na taarifa za mafao mengine au malipo ya vitu; na
•    Kitu kingine kilichotajwa
Kama maelezo yaliyoelezwa hapo juu yamekwisha elezwa katika mkataba ulioandikwa na kupewa mfanyakazi basi mwajiri hana haja ya kumpa mfanyakazi taarifa ya maelezo ya maandishi. Ni jukumu la mwajiri kuhakikisha kwamba maelezo yote au vipengele vya mkataba vinaelezwa katika hali inayoeleweka na mfanyakazi. Ni muhimu kuweka mkataba katika lugha inayoeleweka kirahisi na mfanyakazi, iwe Kiingereza ama Kiswahili. 


Ninaweza kuajiriwa kwa mkataba wa maneno?

Mikataba ya maneno inaruhusiwa; ijapokuwa mfanyakazi ni lazima apewe taarifa ya maelezo ya maandishi  inayoelezea vitu vilivyotajwa hapo juu. Hata hivyo haishauriwi kuingia mkataba wa maneno wa ajira kwasababu itakapotokea suala la taratibu za kisheria jukumu la kuthibitisha ama kukanusha sharti la ajira linalodaiwa litakua ni la mwajiri. Kama mwajiri atashindwa kutoa mkataba wa ajira au taarifa ya maelezo ya maandishi basi atashindwa kuthibitisha sharti lolote lilitojwa na mgogoro unaweza kuamuliwa dhidi yake. Hivyo ni muhimu kumpatia mfanyakazi mkataba wa maandishi au angalua taarifa ya maelezo ya maandishi.

loading...
Loading...