Kusitisha Ajira

Kusitisha ajira maana yake ni kumalizika kwa mahusiano ya kikazi baina ya mwajiri na mwajiriwa au mfanyakazi, kusitisha ajira kihalali, kuachisha kazi isivyo halali, kusitisha kazi kwa makubaliano, mwajiri kusitisha kazi, kuachishwa kazi, kuacha kazi, kustaafu, kuritaya, mwenendo mbaya wa kazi, utovu wa nidhamu sehemu za kazi, kupunguzwa kazi, ridandasi, madhara ya kusitisha kazi isivyo halali, madhara ya kuachisha kazi isivyo halali, fahamu haya kupitia Mywage Tanzania

Kusitisha ajira maana yake ni kumalizika kwa mahusiano ya kikazi baina ya mwajiri na mwajiriwa au mfanyakazi. Kusitisha mkataba wa ajira kunaweza kufanywa na moja kati ya pande mbili, yaani mwajiri au mfanyakazi. Kusitisha ajira kwa kuzingatia sheria kunahusisha yafuatayo:
•    Kusitisha ajira kwa makubaliano: Ni pale ambapo mwajiri na mwajiriwa au mfanyakazi wamekubaliana kumaliza mkataba wa ajira kwa kuzingatia makubaliano. Kwa mfano, kama mkataba ni wa kipindi cha mwaka mmoja na muda huo uliokubalika ukaisha basi mkataba utakua umefikia kikomo.

•    Kusitisha ajira kutokana na mazingira: Mkataba wa ajira unaweza kufikia kikomo kutokana na hali kama kifo au kufa kwa biashara ya mwajiri.

•    Mfanyakazi kusitisha ajira (kujiuzulu): Hii hutokea pale ambapo mwajiri  huvunja vipengele muhimu vya  mkataba na hivyo kupelekea mfanyakazi kuamua kujiuzulu kutoka kwenye ajira yake.

•    Mwajiri kusitisha ajira: Mwajiri pia anaweza kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa kuzingatia sheria na mkataba unaohusiana na kusitisha ajira.


Je mwajiri wangu anaweza kusitisha mkataba wangu wa ajira kwasababu hanipendi?

Hapana, Chini ya sheria kuna misingi minne (4) inayothibitisha kusitishwa kwa ajira na mwajiri, nazo ni:

•    Mwenendo mbaya
•    Kutokua na uwezo wa kufanya kazi
•    Kutokuwiana na wafanyakazi na wateja
•    Mahitaji ya kiuendeshaji ya mwajiri (kupunguzwa kazi)
Mwajiri pia anaweza kusitisha ajira ya mfanyakazi kutokana na kujihusisha katika mgomo usiokua halali. Kwa hivyo kwa mwajiri  kusitisha ajira ya mfanyakazi ni lazima awe na sababu za msingi kama zilivyotajwa hapo juu. Mfanyakazi hawezi kufukuzwa kazi kwasabu mwajiri hampendi isipokua kutokumpenda huku kuwe kumesababishwa na misingi iliyotajwa apo juu kama vile mwenendo mbaya nakadhalika.


Ni zipi sifa za kusitisha ajira kihalali?
Ili kusitisha ajira kuwe kwa halali mbele ya sheria ni lazima kuwe na misingi na kufuata taratibu zilizoainishwa. Mwajiri anahitajika kua na sababu za halali na za haki za kusitisha ajira.
Mbali na sababu hizi za halali za kusitisha ajira, mwajiri ni lazima afuate taratibu za halali za kusitisha ajira kama zinavyoelezwa chini ya sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 na Kanuni za Utendaji Bora za mwaka 2007. Taratibu za kusitisha ajira zinatofautiana kutegemea na sababu za kusitisha ajira lakini zote zina kipengele cha pamoja – Haki ya mfanyakazi kusikilizwa kabla maamuzi ya kusitisha ajira hayajachukuliwa dhidi yake. 


Je ni haki kwa mwajiri wangu kunisitisha ajira papo hapo kama nimefanya utovu wa nidhamu wa hali ya juu kama vile kukamatwa nikiiba?
Bila kujali uzito wa kosa ulilolifanya na bila kujali ushahidi wa kuaminika alionao mwajiri wako, ni lazima kufuata taratibu zilizoainishwa chini ya sheria. Kushindwa kufuata taratibu kunamaanisha mfanyakazi kusitishwa ajira papo hapo bila kupewa nafasi/fursa ya kujitetea mbele ya kamati ya haki ya nidhamu. Ikiwa mfanyakazi hajakiri kutenda kosa basi ni lazima kukaa kikao cha kamati ya nidhamu.
Kusitisha ajira papo hapo ni pale ambapo mfanyakazi hapewi nafasi ya kuwasilisha kesi yake kabla ya kusitishwa ajira. Katika sheria za kazi hii ni sawa na kusitisha ajira isivyo halali. Kuna madhara kadha wa kadha ya kusitisha ajira isivyo halali.

Kama kesi ya jinai juu ya suala tajwa hapo juu imefunguliwa mahakamani dhidi yangu, mwajiri wangu anaweza kusitisha mkataba wangu wa ajira?
Hakuna yoyote anayeweza kusitisha ajira au kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mfanyakazi ambae tayari anakabiliwa na mashitaka hayo mbele ya mahakama ya sheria isipokuwa kama mashitaka hayo ni tofauti au hayatokani na tukio moja.  


Ni yepi madhara yanayoweza kutokana na kusitisha ajira isivyo halali kwa mwajiri?

Kama Tume ya Usuluhishi na Upatanishi au Mahakama ya Kazi itaamua kwamba ajira imesitishwa isivyo halali inaweza kumuamrisha mwajiri afanye yafuatayo:
•    Kumrejesha mfanyakazi kazini toka siku alipositishwa ajira bila ya kupoteza mishahara yake. Hii inamaanisha kwamba mfanyakazi atapewa mishahara yake yote kama vile amekua kazini kwa kipindi chote alichokua amesitishwa ajira. Wakati agizo la kumrudisha kazini linapotolewa lakini mwajiri hataki kumrudisha mfanyakazi, mwajiri atalipa fidia ya mishahara ya miezi kumi na mbili (12) pamoja na mishahara na stahili zote kwa kipindi chote ambacho mfanyakazi hakua kazini mpaka siku ya mwisho ya malipo hayo.

•    Kumrejesha kazini mfanyakazi kutokana na masharti yaliyoamuliwa na Tume au Mahakama. Wakati agizo la kumrejesha kazini linapotolewa na mwajiri hataki kumrejesha mfanyakazi kazini, mwajiri atalipa fidia ya mishahara ya miezi kumi na mbili (12) pamoja na mishahara na stahili zote kwa kipindi chote ambacho mfanyakazi hakua kazini mpaka siku ya mwisho ya malipo hayo.

•    Kumfidia mfanyakazi  si chini ya mishahara ya miezi kumi na mbili (12). Agizo la kufidia litakua ni ziada na si badala ya kiasi chochote ambacho mfanyakazi ana haki ya kupata kwa mujibu wa sheria au makubaliano.

loading...
Loading...