Likizo ya Mwaka

Likizo ya mwaka ni mapumziko ya kazi unayopewa na mwajiri wako huku ukipokea mshahara wako wote, malipo ya likizo ya mwaka, makubaliano ya majadiliano ya pamoja, livu, ruhusa ya likizo, likizo ya dharura, mapumziko ya kaza, fahamu yote kupitia Mywage Tanzania

Ni nini likizo ya mwaka? Ni kwa vipi ninastahili likizo ya mwaka?
Likizo ya mwaka ni mapumziko ya kazi unayopewa na mwajiri wako huku ukipokea mshahara wako wote.  Mfanyakazi au mwajiriwa anastahili likizo ya mwaka kama amemaliza kipindi cha miezi kumi na mbili (12) cha kufanya kazi kwa mwajiri wake. Likizo ya mwaka inakua tayari miezi sita (6) kutoka kuanza kwa ajira na inaweza pia kuchukuliwa kwa misingi ya uwiano. Muda wa likizo ya mwaka ni siku 28 na inajumuisha na mapumziko ya mwisho wa wiki/juma na siku zote za mapumziko kitaifa zitakazoangukia katika likizo.
Likizo ya mwaka inaelezewa katika kipengele D cha sehemu ya tatu (3) ya sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004. 


Mimi ni mfanyakazi wa muda, Je ninastahili likizo ya mwaka?
Ili mfanyakazi aweze kupata likizo ya mwaka ni shurti awe amefanya kazi na mwajiri wake kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12). Kwa maana hiyo hata kama unafanya kazi kama mfanyakazi wa muda, kama kiasi cha kazi kimefikia miezi kumi na mbili (12) una haki ya kupata likizo ya mwaka.
Katika hali fulani sheria inaruhusu malipo ya likizo katika misingi ya uwiano. Kwa mfano, Kama umefanya kazi katika kipindi cha miezi tisa (9) bado unaweza kuwa na haki ya kupata likizo ya mwaka katika misingi ya uwiano. Kiasi cha uwiano cha likizo ya mwaka hukokotolewa kwa makadirio ya malipo (mshahara) ya siku moja kwa kila siku kumi na tatu (13) ambazo mfanyakazi amefanya kazi au alipaswa kufanya kazi. 


Je likizo hii ni lazima ama inaweza kulimbikizwa?
Kwa ujumla, Sheria inapendekeza likizo ya mwaka kuchukuliwa katika mzunguko ule ule wa likizo ya mwaka. Hata hivyo chini ya sheria, mfanyakazi ataomba likizo na ni jukumu la mwajiri kuamua ni wakati gani likizo itachukuliwa. Mwajiri ana uwezo wa kuisogeza mbele lakini isizidi miezi sita baada ya kuisha kwa mzunguko wa likizo ya mwaka au miezi kumi na mbili (12) baada ya kuisha kwa mzunguko wa likizo ya mwaka kama mfanyakazi ameridhia na kusogeza huku ni lazima kuthibitishwe na mahitaji ya kiutendaji.
Katika hali ya kusitisha ajira au kujiuzulu, kama mfanyakazi ana madai au malimbikizo ya likizo mwajiri anawajibika kulipa kiasi hicho.

Ni katika makadirio yepi likizo ya mwaka hulipwa? Je napata malipo yangu yote?
Ndio, unapata mshahara wako wote. Hata hivyo sheria inamuhitaji mwajiri kulipa mshahara wako wote kabla ya kuanza kwa likizo yako. Zaidi ya mshahara wako wa kawaida, agizo la udhibiti wa mishahara na masharti ya ajira la mwaka 2010 linatoa muongozo wa kulipwa malipo kwa ajili ya kusaidia safari kipindi cha likizo na hii hulipwa kila baada ya miaka miwili (2). Dhumuni la malipo haya ni kumsaidia mfanyakazi kujikimu usafiri kipindi cha likizo. Sheria haielezi kiasi kinachotakiwa kulipwa. Mwajiri na mfanyakazi wanatakiwa wajadiliane juu ya kiasi hiki na ama waweke katika Makubaliano ya majadiliano ya pamoja (CBA), Kitabu cha mwongozo cha rasilimali watu au mkataba wa ajira.


Je mwajiri wangu anaweza kunilipa kiasi cha fedha kubadilisha na likizo yangu ya mwaka?

Sheria inakataa kubadilishana likizo na malipo ikiwa mfanyakazi anakubali ama anakataa. Likizo imewekwa ili kumpa mfanyakazi nafasi ya kupumzika ili arudi kazini na akili mpya na nguvu nyingi.
Likizo inalipwa pale tuu ajira inapositishwa/ mfanyakazi kujiuzulu au kufika mwisho wa mkataba na wakati mfanyakazi ana malimbikizo ya siku za likizo.
Vilevile mwajiri haruhusiwi kumwita mfanyakazi kazini kipindi cha likizo. 


Kama nimechukua likizo ya uzazi mwaka huu je nitakua nimepoteza likizo yangu ya mwaka?
Hapana, likizo ya uzazi haiwezi kuondoa likizo yako ya mwaka hata kama zote zitachukuliwa ndani ya mwaka mmoja. Hii ni kwasababu likizo ya mwaka na likizo ya uzazi zina madhumuni tofauti. Kifungu cha 31 (5)kinaeleza kwamba mwajiri haruhusiwi  kutoa likizo ya mwaka pale ambapo mfanyakazi ana haki ya likizo nyingine kama vile likizo ya uzazi nakadhalika. 


Kama kuna dharura inayonihitaji kupumzika kazi bila makato, je bado nina haki na likizo yangu ya mwaka?

Ndiyo. Kama umepumzika siku kadhaa bila makato katika mzunguko wa likizo bado una haki ya likizo yako ya mwaka ikiwa pungufu ya siku ulizopewa kupumzika baada ya kuomba.

Loading...