Kazi na Familia

Fahamu zaidi kuhusu sheria za kazi za Tanzania zinazungumzia nini kuhusu kazi na familia, je sheria zinatoa nafasi kwa wafanyakazi kushiriki katika shughuli za familia? Fahamu yote haya na zaidi kupitia www.mywage.org

Je,sharia inasemaje kuhusu wazazi wanaofanyakazi?
Sheria za kazi kwa sasa nchini Tanzania hazijatoa msimamo maalum kuhusiana na wazazi wanaofanyakazi.Hatahivyo kuna msimamo kuhusu wajawazito na wale wanaonyonyesha.


Je, sheria inasemaje kuhusu wanawake wajawazito na muda wa kufanya kazi?
Sheria inakataza wanawake wajawazito kufanya kazi usiku kabla ya muda wa kwenda mapumziko au mapema sana endapo mhusika ataonesha cheti cha daktari kinachothibitisha kuwa hana nguvu ya kufanya kazi usiku.  Sheria iko wazi kuhusu kipengele kinachomtaka mwajiri kumhamisha mtumishi kutoka muda wa usiku hadi muda mchana inapobainika kuwa hawezi kufanya kazi usiku.


Je, sheria inasemaje kuhusu likizo ya uzazi kwa mke na mume?
Katika mzunguko wa likizo (kipindi cha miezi36) mtumishi wa kike ana haki ya kupewa siku 84 za likizo ya malipo iwapo atajifungua mtoto mmoja au siku 100 za likizo ya malipo iwapo atajifungua mtoto zaidi ya mmoja.  
Siku hizi hujumuisha siku za mapumziko na zile za sikukuu za kitaifa. Hata hivyo endapo mama mjamzito atahitaji siku nyingi zaidi kutokana na matatizo, anaweza kujadiliana na mwajiri wake, kuhusu kutumia siku za likizo ya kuugua au siku chache kutoka kwenye zile za likizo ya mwaka.
Likizo ya uzazi kwa mwanaume ni siku tatu katika kipindi cha miezi 36. Siku tatu hutolewa bila kujali idadi yawatoto waliozaliwa katika kipindi cha likizo.


Je, mama mjamzito ana haki ya kupewa muda wa kwenda kliniki kabla na baada ya kujifungua?
Sheria haina kipengele kinachoeleza wazi wazi kuhusu muda wa kwenda kliniki kabla na baada ya kujifungua. Uzoefu unaonesha kuwa kwa kawaida mama mjamzito au mkunga anayetaka kwenda kliniki, au anayehitaji tiba ya afya anatakiwa kuomba siku chache kutoka kwenye siku za likizo ya afya au likizo ya mwaka. Hata hivyo, baadhi ya makampuni, yana makubaliano sawa au sera ya mahali pa kazi inayotoa siku chache za kwenda kwenye matibabu kabla na baada ya kuzaa.


Je, sheria inasema nini kuhusu muda wa kufanya kazi kwa mama anayenyonyesha?
Mama anayenyonyesha hupewa masaa mawili kisheria ya kwenda kunyonyesha mtoto. Sheria haisemini wakati gani muda huo utumike. Hivyo basi ni wajibu wa mwajiri na mtumishi kujadili na kukubaliana wakati wa kwenda kunyonyesha. Sheria pia haioneshi ni kwa muda gani haki hiyo itaendelea, hivyo suala hili limeachiwa mwajiri na mtumishi kujadilina kufikia makubaliano.


Je, kuna kipengele chochote kinachotoa likizo ya kwenda kumsaidia mgonjwa au kushughulikia masuala ya kifamilia?
Ndio. Kuna kipengele cha likizo ya huruma na hii humsaidia mtumishi anayekwenda kumsaidia mtoto anayeumwa au kwenda kuzika mtoto aliyefariki dunia. Sheria hii pia hutoa fursa kwa mtumishi kwenda kuzika mke au mume, mzazi, mababu na mabibi, wajukuu na ndugu wa kuzaliwa nao.
Idadi ya siku ambazo mtumishi hupewa wakati wa likizo ya dharura ni siku nne katika kipindi cha miezi thelathini na sita. Hatahivyo, watumishi wamekuwa wakilalamika kuwa siku hizo hazitoshi baadhi wameweza kuongeza siku hizo kwa njia ya majadiliano.


Je, sheria inanipa muda wa mapumziko ilikujihusisha na masuala ya kifamilia au ya kijamii?
Sheria haina kipengele anuai kwa ajili ya masuala ya familia/mihadhara ya kijamii au shughuli za aina hiyo. Hata hivyo, endapo mtumishi anahitaji muda wa kupumzika, tuseme kwenda kuhudhuria harusi ya bintiye au mazishi y ashangazi yake, wanaweza kuomba wakatwe siku hizo kwenye likizo ya mwaka.


Je, ni changamoto zipi zinazowakabili wazazi wanaofanya kazi?
Kuna changamoto nyingi zinazowakabili wazazi wanaofanya kazi.Suala kubwa ni kuwa hawapati muda wa kukaa na familia, kufanya kazi za nyumbani, na kuhudhuria shughuli za kijamii. Pia kusafiri kuna kula muda mwingi kutokana na miundombinu mibovu, ni jambo la kawaida kwa wazazi kutoka nyumbani saa 10 alfajiri nakurudi saa 3 usiku. Kwa muda kama huu ni vigumu kwa mzazi kukaa na familia.

loading...
Loading...