Mafao ya Kusitisha Ajira

mafao ya kusitishwa ajira, mafao ya kufutwa kazi, ajira, mafao ya kuachishwa kazi, kiinua mgongo, malipo ya usafiri kwenda mahali ulipoajiriwa,stahili za kuachishwa kazi, fahamu yote haya kupitia Mywage Tanzania

Ni yapi mafao ya kusitisha ajira?
Mafao ya kusitisha ajira ama kuachishwa kazi ni haki/stahili zote anazotakiwa apate mfanyakazi kutokana na kuisha ama kusitishwa kwa mkataba wa ajira.
Ni yepi ninayostahili kama mafao ya kuacha kazi baada ya kusitisha ama kufikia mwisho wa mkataba wa ajira?
Kwa ujumla kifungu cha 44 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 inaeleza baada ya kusitisha ajira ama kufikia mwisho wa mkataba wa ajiramwajiri atahitajika kfanya yafuatayo;
•    Ujira wowote wa kazi iliyofanyika kabla ya kuachishwa kazi;
•    likizo yoyote ya mwaka inayodaiwa na mfanyakazi kwa likizo ambayo mfanyakazi hajachukua;
•    malipo yoyote ya likizo ya mwaka iliyopatikana wakati wa mzunguko wa likizo usiokamilika
•    malipo yoyote ya notisi.
•    malipo yoyote ya kiinua mgongo yanayodaiwa
•    Posho yoyote ya usafiri ambayo inaweza kuwa inadaiwa
•    Baada ya kuachishwa, mwajiri atatakiwa kumpa mfanyakazi cheti maalumu cha utumishi
Hayo yaliyoelezwa hapo juu ndio yanayojulikana kama mafao ya kuacha ama kuachishwa kazi; ijapokua hayatolewi moja kwa moja. Hii inamaanisha hutolewa kwa kuzingatia mazingira tofauti kama vile sababu za kuachishwa kazi, aina ya mikataba ya ajira, muda wa utumishi kwa mwajiri nakadhalika. 


Je mwajiri anaweza kuninyima kiinua mgongo kama nimeachishwa kazi kutokana na mwenendo mbaya?
Kutokana na Sheria ya Ajira na Mahusiano ya kazi ya mwaka 2004 inaeleza kua mfanyakazi hatokua na haki ya kupata kiinuo mgongo kama ataachishwa kazi kutokana na mwenendo mbaya. Pia mwajiri hatomlipa mfanyakazi kiinuo mgongo kama mfanyakazi ataachishwa kazi kutokana na uwezo wa kufanya kazi ama mahitaji ya kiundeshaji ya mwajiri na kukataa ajira mbadala bila sababu za msingi.
Kigezo kingine cha mfanyakazi kulipwa kiinua mgongo ni lazima awe amefanya kazi kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12) mfululizo na mwajiri na kuachishwa kwake kazi kuwe kumeanzishwa na mwajiri. 


Je nitapata kiinua mgongo baada ya kustaafu?
Kutokana na marekebisho ya hivi karibuni ya kifungu cha 42 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya kazi ya mwaka 2004, mfanyakazi aliyestaafu ajira hastahili kiinua mgongo. Hii inatokana na mantiki kwamba mstaafu hupokea pensheni kutoka kwenye mfuko wa pensheni alipokua mwanachama. Marekebisho haya yapo katika sehemu ya V ya sheria ya marekebisho ya sheria Na 3 ya mwaka 2010. Kwa ivyo hutostahili kiinuo mgongo pale utakapostaafu bali utapata pensheni kutoka mfuko wa pensheni. Hali nyingine ambayo inaweza kupelekea kutokulipwa kiinua mgongo ni pale ambapo mfanyakazi amefanya kazi chini ya mkataba wa kudumu na muda wa mkataba ukaifikia mwishoni. 


Ni vipi kiinua mgongo hukokotolewa?
Kiinua mgongo kinamaanisha kiasi angalau sawa na mshahara wa siku saba kwa kila mwaka uliofanya kazi na mwajiri kwa kipindi kisichozidi miaka kumi. Hivyo katika kukokotoa kiinua mgongo unazidisha mshahara wa siku saba kwa idadi ya miaka ambayo mfanyakazi ametumikia isiyozidi miaka kumi (10). 

Ni nini notisi ya kusitisha ajira? Ni vipi inatolewa? Je ni lazima?
Notisi ya kusitisha ajira ni taarifa inayotolewa na upande mmojawapo (mwajiri au mfanyakazi) katika mkataba wa ajira inayoeleza nia ya upande mmoja kusitisha mkataba wa ajira katika wakati fulani. Kipindi cha kutoa taarifa kinatofautiana katika njia zifuatazo:
Kama taarifa ya kusitisha ajira itatolewa katika mwezi wa kwanza wa ajira basi muda wa kutoa taarifa usipungue siku saba (7). Katika muda huo mfanyakazi atatakiwa kuendelea kufanya kazi kutoka siku ametoa taarifa juu ya kusitisha ajira ama amepokea taarifa juu ya kusitishwa ajira mpaka siku ya mwisho ya kufanya kazi kama taarifa itakavyoeleza.
Kama mfanyakazi ameajiriwa kwa siku ama kwa wiki basi muda wa kutoa taarifa ni siku nne (4) na kama mfanyakazi ameajiriwa kwa mwezi basi muda wa kutoa taarifa ni siku 28. Mkataba wa ajira unaweza kuruhusu muda zaidi wa kutoa taarifa lakini muda huo ni lazima uwe sawa kwa mwajiri na mfanyakazi. Notisi ya kusitisha ajira ni lazima ieleze sababu ya kusitisha ajira na tarehe ambayo notisi imetolewa.

Je sheria inaruhusu mwajiri kunifukuza kazi bila kuniruhusu kufanya kazi kipindi cha notisi?
Pale ambapo mwajiri anataka kusitisha ajira ya mfanyakazi bila kumruhusu kufanya kazi katika kipindi cha notisi basi mwajiri anahitajika kumlipa mfanyakazi kiasi ambacho mfanyakazi angepata kama angefanya kazi kipindi cha notisi. Hii kwa kawaida inajulikana kama malipo badala ya notisi.
Kama mfanyakazi atakataa kufanya kazi wakati wa kipindi cha notisi, mwajiri anaweza kukata kutoka kwenye fedha yoyote inayodaiwa na mfanyakazi huyo wakati wa kusitishwa ajira, kiasi ambacho kingedaiwa na mfanyakazi kama mfanyakazi huyo angefanya kazi wakati  wa kipindi cha notisi.


Nimesitishwa ajira na mwajiri wangu hataki kugharamia usafiri wangu, je hii ni sawa kisheria?
Pale ambapo mkataba wa ajira umesitishwa mahali mbali na pale ulipoajiriwa basi unastahili kusafirishwa wewe pamoja na vitu vyako mpaka mahali ulipoajiriwa. Kwa mfano mfanyakazi amejiriwa Dodoma na kisha kuhamishiwa kwenye tawi la ofisi ya Arusha, kama atasitishwa ajira akiwa Arusha mwajiri atalazimika kumsafirisha mfanyakazi hadi Dodoma alipoajiriwa. Mwajiri atachagua kati ya haya:
•    Kumsafirisha mfanyakazi na vitu vyake kwenda sehemualiyoajiriwa;
•    Kulipa gharama za usafirishaji wa mfanyakazi kwenda mahali alipoajiriwa; au
•    kumlipa mfanyakazi posho ya usafiri kwenda sehemu aliyoajiriwa kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2) na posho ya gharama kwa kila siku wakati wa kipindi, kama kipo, kati ya tarehe ya kusitishwa kwa mkataba na tarehe ya kumsafirisha mfanyakazi na familia yake kwenye sehemu aliyoajiriwa. 


Je inakuaje kama nimesitishwa ajira wakati ninadai likizo ambazo sikuchukua?
Inapotokea mfanyakazi amelimbikiza likizo mwajiri atalazimika kumlipa mfanyakazi wakati wa kusitisha ajira katika misingi ya uwiano kiasi cha fedha badala ya likizo ya mwaka ambayo mfanyakazi anastahili, kwa kuzingatia kwamba itachukuliwa si chini ya miezi sita (6) baada ya kumalizika mzunguko wa likizo au miezi kumi na mbili (12) baada ya kumalizika mzunguko wa likizo ( kama mfanyakazi ameafiki au kuzidishwa huku kunaelezewa na mahitaji ya kiundeshaji). Kama kushindwa kuomba likizo kulitokana na uzembe wa mfanyakazi basi mfanyakazi hatostahili malimbikizo ya likizo. 


Je cheti cha utumishi na notisi ni lazima hata kama kusitishwa ajira kunatokana na mwenendo mbaya?
Ndio, notisi na cheti cha utumishi ni lazima bila kujali sababu ya kusitishwa ajira.

Loading...