Usalama wa Ajira

This page was last updated on: 2023-05-18

Hati ya Maandishi ya Ajira

Mkataba wa ajira ni mkataba, uwe umeandikwa au umetamkwa, kati ya mwajiri na mfanyakazi ambapo mfanyakazi anakubali kumfanyia kazi mwajiri ili apate mshahara.

Huenda mkataba wa ajira ukawa kazi ya kudumu (kwa kipindi cha muda usiojulikana), kazi ya muda (kwa kipindi kinachojulikana), kazi ya muda maalum na kazi ya kila siku. Huenda mwajiri akaandika mkataba wa ajira na mfanyakazi ambaye amefanya kazi na mwajiri huo kwa kipindi kinachoendelea cha miezi sita ikiwa mwajiri bado anahitaji huduma za mfanyakazi huyo. Ni kinyume cha sheria kumwajiri mfanyakazi anayelipwa kila siku kwa kazi ambayo ni ya kudumu.

Mkataba wa muda unaweza kuwepo kwa kipindi cha miezi sita hadi miaka mitatu. Waziri wa Kazi anaweza kutoa sheria inayobainisha kategoria maalum za huduma na wafanyakazi ambao wanaruhusiwa kufanya kazi chini ya mkataba wa muda wa huduma. Mkataba wa ajira wa kipindi kinachozidi miezi sita lazima uandikwe. Mikataba ya kipindi kifupi inaweza kutamkwa na mkataba wa kutamkwa huisha ikiwa mfanyakazi bado anahitaji huduma za mfanyakazi baada ya miezi 6. Mwajiri anahitajika kutoa nakala ya mkataba wa ajira kwa mfanyakazi ajira inapoanza. Mfanyakazi anahitajika pia kuhakikisha kwamba mfanyakazi anaelewa masharti yote ya mkataba wa ajira. Mfanyakazi, anapokuwa akiingia katika uhusiano wa kikazi, lazima afanyiwe vipimo vya kimatibabu kwa gharama yake mwenyewe na alete ripoti hiyo ya matibabu inayo ashiria kwamba anafaa na anaweza kuajiriwa katika huduma inayohitajika. Kila mkataba unaoandikwa wa ajira lazima uthibitishwe na afisa wa kazi. Sheria ya Ajira inahitaji kwamba mkataba wa ajira kwa ajira nje ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania na hata pia mkataba na mfanyakazi wa kigeni anayetaka kuajiriwa Tanzania lazima uandikwe. Sheria ya Ajira inabainisha pia vipengele fulani ambavyo lazima viwe sehemu ya mikataba hii iliyoandikwa kama vile majina na vyombo vya wahusika, hali ya kazi, kipindi cha ajira, mishahara na marupurupu, mishahara, marupurupu na livu ya kila mwaka, n.k.

chanzo: §43-48 & 56-57 ya Sheria ya Ajira Nambari 11 ya 2005

Mkataba wa kazi wa kipindi maalumu

Sheria ya Kazi inapiga marufuku kuwaajiri wafanyakazi kwa mkataba wa muda uliowekwa kufanya kazi ya hali ya kudumu. Sheria ya Ajira huchukulia pia kuwa hatia kumwajiri mtu kama mfanyakazi anayelipwa kila siku katika ajira ya hali ya kudumu.

Mkataba wa muda unaweza kuwepo kwa kipindi cha miezi sita hadi miaka mitatu. Kwa hivyo, muda wote wa mikataba ya muda uliowekwa pamoja na kubadilishwa (haujabainishwa waziwazi chini ya sheria) ni miezi 36. Waziri wa Kazi anaweza kutoa sheria inayobainisha kategoria maalum za huduma na wafanyakazi ambao wanaruhusiwa kufanya kazi chini ya mkataba wa muda wa huduma.

chanzo: §44 & 45.2 ya Sheria ya Ajira Nambari 11 ya 2005

Kipindi cha majaribio kazini

Kipindi cha Majaribio humruhusu mwajiri kutathmini ujuzi wa mfanyakazi katika kazi yake, hasa kuhusiana na ustadi wake, na mfanyakazi kuamua kama kazi mpya inamfaa.

Kipindi cha majaribio cha mfanyakazi mwenye mkataba wa kudumu ni miezi 06 kuanzia tarehe ya kuajiriwa. Kipindi hiki cha majaribio kinaweza kuongezwa kwa miezi 06 (jumla ya miezi 12). Kwa mfanyakazi mwenye mkataba wa muda wa ajira wa kutamkwa (ambayo inamaanisha chini ya kipindi cha miezi sita), kipindi cha majaribio ni miezi 03. Mwisho wa kipindi hicho cha majaribio, mfanyakazi anachukuliwa kuwa amethibitishwa iwe barua ya kuthibitisha imetolewa na mwajiri au la. Wakati wa kipindi cha majaribio, mhusika yeyote anaweza kukatisha mkataba wa ajira kwa kumpa yule mwingine notisi ya siku 14 au kulipia badala ya ilani hiyo.

Ujauzito au kumnyonyesha mtoto na kutokuwepo kazini kwa sababu ya mfanyakazi kuwa mgonjwa hakupaswi kuzingatiwa kuwa sababu nzuri ya kukatisha mkataba wa ajira wakati wa kipindi cha majaribio.

chanzo: § 65 ya Sheria ya Ajira Nambari 11 ya 2005

Loading...